Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani kanda ya Afrika alifariki dunia alipokuwa akipokea matibabu nchini India, spika wa bunge la Tanzania alisema Jumatano.
Mipango ya kurejesha mwili wa Dk. Faustine Ndugulile, 55, inaendelea, Spika Tulia Ackson aliambia shirika la habari la AP na kuongeza kuwa mipango ya mazishi itatangazwa baadaye. Hakufichua maradhi yaliomsibu Ndugulile.
Ndugulile aliwahi kuwa mbunge wa Jimbo la Kigamboni katika mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania, Dar es Salaam. Pia alikuwa naibu waziri wa afya kati ya mwaka 2017-2020 na waziri wa habari na mawasiliano hadi 2021.
Alichaguliwa kuwa mkurugenzi wa Afrika wa WHO mwezi Agosti na alitazamiwa kuanza jukumu lake jipya Februari 2025, kufuatia Dkt. Matshidiso Moeti ambaye alihudumu katika jukumu hilo kwa mihula miwili.
Katika hotuba yake ya kukubali uteuzi, Ndugulile alieleza dhamira thabiti ya kuendeleza afya na ustawi wa watu barani Afrika.